HALLELUJAH

BWANA YESU KRISTO ASIFIWE! Nakusalimu mtu wa Mungu. karibu katika ukurasa huu maalumu kwa ajili ya mafundisho ya Neno la Mungu, naamini utajifunza na kujengeka kiroho.

"Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkishukuru Mungu Baba kwa yeye."
wakolosai 3;16,17

Wednesday, 24 August 2016

MAMBO YA KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYAUAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA

MAFUNDISHO MAALUM KWA VIJANA

By
Mwalimu Christopher Mwakasege
Wiki ya Nane
Jambo la Nane; “Je! Uko tayari kuolewa na nani”
Wengine hawafikirii namna hiyo, ukiwauliza uko tayari kuolewa na nani, anasema na mtu
aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri, unataka kuolewa na nani.
Labda hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo, nataka nikufikirishe vitu vya kawaida kabisa.
Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na mtumishi, hesabu gharama kwanza! Wengine wanaona tunavyoshirikiana na mke wangu katika huduma wanamtazama wanasema, wanataka kuolewa na mtumishi; kaamuulize mke wangu, tulipokutana hata wito haukuweko, na tulikutana wote hatujaokoka. Tulikuja kuokoka baada ya kuoana! Mungu ametuteremshia utumishi tuko kwenye ndoa tayari, kwa hiyo usitamani ndoa ya kwetu, tamani ya kwako ambayo Mungu amekupangia. Mke wangu hakunipendea utumishi, sikuwa na tone la utumishi, wala hata ya kufanania ya kwamba nitaokoka, na yeye  alikuwa hajaokoka pia wakati huo. Lakini kwa saa na kwa makusudi na kwa utaratibu wa Mungu, tumekuwa jinsi tulivyo. Akatuteremshia utumishi wakati tumekwishaokoka na tumekwishaoana!
Usijaribu kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu mwingine, hujui iliko toka, tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka mtumishi, lakini watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna gani? Lazima ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka mhubiri,
hata nabii ni mhubiri, mwinjilisti ni muhubiri, mwalimu anaweza akahubiri. Kitabia hawafanani, haleluya! Nataka nikufikirishe ikusaidie, maana nataka nikujengee msingi mzuri wa maisha ambao ukikanyaga vizuri shetani alie tu, maana hatawezi kukuvuruga.
Maana watu wengi wanapata shida sana wanapotaka kuoa au kuolewa, utakuta wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na mtumishi, hayo ni maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya
Roho Mtakatitu, bado yuko chekechea, unajua lazima uwe ‘very specific’. Mungu anataka useme naye kile kitu unachokisikia ndani yako. Anajua kabisa kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yako; lakini Mungu hataki kukulazimishia tu, anataka ushirikiane naye, ili akikupa kitu ukipokee kwa furaha.
Kwa hiyo kama unataka mtumishi, ni muhimu useme unataka mtumishi wa aina gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu gharama, lazima uwe na neema ya kukaa na mwinjilisti.
Si unajua mwinjilisti hakai nyumbani, anazunguka, akikosa watu wa kuwachapa injili huko nje, anakuja kuchapa injili nyumbani hata kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi kumaliza ibada ya jioni mpaka awepo mtu wa kutubu, hajatubu ataendelea kufanya maombi. Kama hauko tayari kuchukuliana na mtu wa namna hiyo usiamue kuoa au kuolewa naye.Lazima useme; au kama unataka kuolewa na nabii jipange, kwa sababu hajui kuongea na watu, muda wake mwingi yuko kimya, manabii mara nyingi wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya. Mara nyingi amejifungia kuomba peke yake na Mungu. Hata saa nyingine unatamani
uombe pamoja naye, lakini Mungu anataka yeye peke yake. Wewe nenda kwenye biblia utaona maisha yake yalivyo kila kitu kinachomzunguka, kila kitu anachovaa, kila kitu anachokutana nacho,
Mungu anaweza akakigeuza ujumbe. Kwa hiyo usije ukashangaa kesho akakutazama na akaishia kupata mahubiri toka kwako, halafu mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na unamuuliza sasa wewe ulikuwa unanihubirije?

Kwani wewe hukujua ya kwamba ni nabii na anaweza kupata ujumbe unaosema: “kama vile mke wako alivyovaa, ndivyo na kanisa langu lilivyo asema, Bwana”! Wewe usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na anaona jinsi mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu, “kama vile mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto, ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili ya watoto wangu, asema Bwana”! Saa nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani vinaonekana, ujumbe unatoka saa hiyo mara moja, anasema, “Kama vile mke wako alivyovaa nguo iliyopasuliwa na watu wanaona ndani, ndivyo na kanisa langu lilivyo vazi lake limepasuliwa na shetani anaona ndani”! Lazima uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na nabii. Uwe tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii! Unataka kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea wageni. Mwingine anasema mimi ninataka kuolewa na mtumishi lakini ndani yake anawaza mtu anayezunguka na kuhubiri, kumbe Mungu ameweka ndani yake mtumishi, lakini ni mfanya biashara. Mfanya biashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio sehemu yake kumtumikia Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni dereva, wanapakwa mafuta sehemu zao hizo za utumishi, usije ukafikiri hao wanaoafanya kazi nyingine sio watumishi wa Mungu. Mungu anawapaka mafuta kwa ajili ya hizo kazi, ili walitumikie kusudi lake. Kwa hiyo unapokwenda katika maombi unasema tu mimi ninaomba mtumishi, Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine wanafagia barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye vyoo vya kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha nyumba za watu, nao ni watumishi wa Mungu,oh haleluya! Mungu akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi sikuomba huyu niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu, usimnenee kitu cha namna hiyo. Kama msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu, au kijana ni mrefu unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi kukupa, lakini wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine anakuwa mfupi kiasi ambacho anafanana kama vile ni mtoto kwako, wenzako wanakuuliza tangu lini umepata mtoto na akakua na akawa mkubwa namna hii, unasema “ninyi msiseme hivyo, ni mume wangu huyu”. Ni uamuzi wako. Sasa, si lazima mfanane urefu, lakini msipishane sana; kwa kweli ni kwa faida yenu wenyewe, haleluya!Kama msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana unaweza ukapata mtumishi wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe huzitaki. Ikifika siku umeingia tu kwenye ndoa kitu cha kwanza unamtafutia wembe ili anyoe ndevu zake – hii ni kumwonea! Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe wewe ulikuwa unamtegea tu ili baada ya arusi tu umpe wembe! Wako wasichana wanaopenda wanaume wenye ndevu, waachie hao! Huyu Bwana Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa ninawaza jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na nabaki ninashangaa sana. Maana kuna wanaume wengine hata ndevu hawana, hata wakilazimishia kunyoa kidevu kitupu haziji. Sasa mtu mwingine anajisikia vibaya, akifikiri ya kuwa mtu anaonekana ya kwamba yeye ni mwanaume kwa sababu tu ana ndevu, si kweli. Kuna wanaume wengine wametengenezwa namna hiyo ‘special’ kwa ajili ya wasichana wasiotaka wanaume wenye ndevu, haleluya! Maana mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka karibu na kwenye pua. Sasa kama ni mtu mweusi sana ‘ni hatari sana’, giza likiingia tu ndani ya nyumba wewe unamwambia ‘cheka’, akicheka yale meno yake yanaweza yakamulika kidogo, na utajua yuko wapi! Hivi vitu ukishaingia kwenye ndoa ni vitu vikubwa sana, kuliko watu wanapoviangalia kabla hawajaoana. Wewe unakuta kijana anaoa msichana ana rangi nyeusi nzuri tu, akifika ndani unamletea madawa ajikoboe, wewe ulikuwa unamwoa wa nini? Hiyo sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli nimechukua tu huyu, lakini sio niliyekuwa namtaka! Niliyekuwa namtaka ni mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha nimkoboe mpaka afike rangi ninayotaka, - haviendi namna hiyo bwana! Mungu alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo aliona, alimtazama alivyo na weusi wake huo akaona kila kitu chema, akajipa sifa, akajipa maksi asilimia mia moja, amefanya kitu chema! Sasa akitaka kupaka rangi hiyo ‘nyumba yake’ na kuinakshi ni kitu kingine. Unajua kuna nyumba nyingine hazipendezi mpaka uzipake rangi fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine hawawezi kupendeza mpaka wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa utapata mtihani mgumu, nimeona, kijana anampenda msichana, lakini msichana anaweka rangi kwenye midomo yake, kucha zake anaweka rangi, anachora na kalamu hapa kwenye nyusi kidogo, ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu kingine juu ya uso wake. Umempenda akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia hukumuuliza hayo maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo rangi! Hiyo ni kumwonea, maana ulimkuta akiwa hivyo, kama ulikuwa humtaki akiwa amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa kumfuatilia, wako wengine ambao watakuwa radhi na huyo anayejipaka rangi! Kuna kijana alioa msichana, wamefika ndani wakaanza kugombana naye habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, - nywele tu! Huyu dada kaenda katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki. Lakini alimkuta yule msichana anatengeneza nywele kwa staili hiyo, sasa kwa nini hivi vitu hawakutaka kuzungumza kabla ya kuamua kuoana? Mimi ninataka nikusaidie upunguze ugomvi ndani ya ndoa utakayokuwa nayo; maana vitu ambavyo Mungu atawaletea vya kufanya pamoja kwenye ndoa ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi ambacho hamhitaji kutumia muda wenu kushindania vitu vidogo vidogo ambavyo mlikuwa muwe mmekwisha kuvijadili kabla ya kuoana. Mna mambo muhimu sana ya kufanya, kiasi ambacho kuanza kushindana na kubishana juu ya vitu ambavyo mlitakiwa muwe mumeshavizungumza kabla ya kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa Mungu ulivyo juu ya kumpata mwenzi wa maisha.

1 comment:

Unknown said...

AMINA nimepata vitu vingi mnooo barikiwa sana Baba

Popular Posts

Pageviews

WASILIANA NASI

Name

Email *

Message *