HALLELUJAH

BWANA YESU KRISTO ASIFIWE! Nakusalimu mtu wa Mungu. karibu katika ukurasa huu maalumu kwa ajili ya mafundisho ya Neno la Mungu, naamini utajifunza na kujengeka kiroho.

"Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkishukuru Mungu Baba kwa yeye."
wakolosai 3;16,17

Wednesday, 24 August 2016

MAMBO YA KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYAUAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA

MAFUNDISHO MAALUM KWA VIJANA
By Mwalimu Christopher Mwakasege

Wiki ya Kumi
Jambo la Kumi; Uko tayari kuzaa, kutunza na kulea watoto wangapi?
Niliuliza vijana fulani ambao ndio wametoka tu
kuoana, wanafurahia maisha yao, ghafla nikawauliza swali ambalo hawakutegemea, nikawauliza, “mna mpango wa nakuzaa watoto wangapi? Walinitazama wakasema, “Mungu anajua”. Nikawambia; “siyo hivyo! Mungu anajua lakini ninyi je?” “Wakasema hatujui”, nikawaambia hayo ndio makosa ya wengi waliomo katika ndoa. Sasa ninakueleza hivi kwa sababu ni vitu ambavyo Mungu alisema na sisi mapema. Hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kuokoka ambaye sikujua ya kwamba atazaliwa, na hakuna mtoto aliyezaliwa baada ya sisi kukuokoka ambaye sijajua wito wake. Na Mungu aliponyamaza na hakutuonyesha mtoto mwingine, hatukuona sababu ya sisi kutafuta  mtoto mwingine.
Wengine wanafikiri Mungu hana mipango ya uzazi (kasome biblia yako vizuri) – Mungu ana utaratibu wa uzazi kwa kila ndoa anayoisimika.Ni kitu ambacho unahitaji kuomba, ili Mungu akujulishe. Nimeona watu wakishindana ndani ya ndoa, baba anataka watoto wengi, mama hataki. Nimekuta ndoa nyingine mama anataka watoto wengi wamzunguke kama timu ya mpira lakini baba hataki. Na ugomvi mkali unatokea juu ya hili.
Mwingine anamzalisha mke wake kila mwaka (unaelewa maana ya kila mwaka?) si unaelewa mimba inakaa miezi tisa tumboni, kwa hiyo anaweza akazaa kila mwaka! Sasa umewahi kufikiri kila mwaka unazaa, kwa hiyo ikiwa uko kwenye ndoa miaka kumi basi una watoto kumi. Au mtu yuko kwenye ndoa miaka mitano, tayari ana watoto wanne na bado anaendelea kuzaa – hii ni sawa?
Nilikwenda mahali fulani kwa ajili ya huduma dada mmoja alikuwa anafurahia muujiza wake wa tumbo, jinsi ambavyo Mungu amemponya, akasema, “sasa nitakuwa tayari kuzaa mtoto mwingine”. Nikamuuliza, “una watoto wangapi sasa?” Akasema, “wanne”. Nikamwambia, “Na bado unahitaji mtoto mwingine”. Akasema, “ndio, ninataka mtoto mwingine”! Unajua kwa nini ninakueleza vitu vya namna hii, - kwa sababu kila mtoto ana wajibu wake, ana mzigo wa kwake na anatunzwa kivyake!
Kadiri unavyozaa watoto wengi, ndivyo unavyozidi kuwa na wajibu mkubwa zaidi wa kulea. Watoto hawafanani, huwezi ukawalea kijumla. Watoto hawalelewi kwa namna hiyo. Kila mtoto ameitwa kivyake, ana mpango wake, ana njia yake, ana tabia yake na ana namna yake ya kutunzwa,– hawafanani!Mtoto anayezaliwa lazima umlee kwa uangalifu. Hujamfikisha mahali katika kumlea, tayari ameshakuja mwingine, unafikiri mchezo!Hao watoto wawili hujawafikisha mahali katika kuwalea tayari ameshakuja mwingine, ni kitu kigumu hujawahi kuona! Huyu wa kwanza hapati tena ule umuhimu wake na nafasi yake, kwa sababu sasa anakimbiliwa huyu aliye mdogo; akija mwingine anakimbiliwa aliye mdogo zaidi, hao waliotangulia wanajikuta wanakua kivyao.
Watu wengi wanabaki kushangaa kwa nini watoto wengi waliozaliwa kwa kufuatana saa nyingine kwa karibu wanagombana. Ni kwa sababu huyu mkubwa anaona ameingiliwa na huyu mdogo, na huyu mdogo anaona kwamba huyu mkubwa ameshakuwa mkubwa, kwa hiyo mimi niliye mdogo ndiye mwenye haki zaidi. Ni ugomvi unaoweza ukaendelea mpaka wamekuwa watu wazima.
Mimi nimesoma masuala ya uchumi, sijasomea masuala ya kuhubiri. Si kwa sababu sikupenda kusomea kuhubiri, lakini hakuwa mpango wa Mungu wa kunilea namna hiyo katika wito. Kuna wengine Mungu anawapanga na kulea wito wao kwenye vyuo vya biblia; na ni mpango wa Mungu tu mzuri. Lakini Mungu alikuwa na mpango mwingine na mimi. Mimi katika chuonilikwenda kusoma masuala ya uchumi.
Sasa, siku moja nchi hii ilitembelewa na wageni, wa kutoka Washington D.C, wa shirika la fedha ulimwenguni. Wale watu wakatuuliza maswali, hebu tuambieni mabadiliko ya uchumi yanayoendelea hapa nchini ninyi mnayaonaje.
Mama mmoja akanyoosha mkono, akasema, “Tunaelewa umuhimu wa mabadiliko mengine yanapotokea katika uchumi wa nchi, kwa sababu ya mazingira tunayoyaona hasa tunapoona vitu vingine havifanyi kazi. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kubadilisha sera zingine ili mambo yaende
sawasawa. Lakini tatizo tulilonalo, ni kwamba maandalizi ya kutuandaa sisi kama watanzania ya kwamba kuna mabadiliko yanakuja, hayo maandalizi hayajafanyika ya kutosha”. Wakasema, “mama tupe mfano”. Akasema “kwa mfano, tunatakiwa kuchangia masuala ya afya, tunatakiwa kuchangia masuala ya elimu, kama tungejua kwa mfano, miaka mitano au sita kabla, kwamba miaka sita ijayo au miaka kumi ijayo, ya kuwa pamoja na kwamba sasa elimu ni bure, afya ni bure, iko siku mtahitaji kutoa pesa zenu mfukoni ili kulipia gharama hizi – tungekuwa waangalifu tunazaa watoto wangapi.”
Nikagundua mara moja kwamba huyu mtu wazo lake lilikuwa ni zuri kabisa.Kwa sababu kwa watanzania wengi inapofika mtoto anazaliwa walijua anayewajibika kumpeleka huyo mtoto shule ni serikali, anayewajibika kumlipia gharama za hospitali ni serikali! Wewe utazaaje ili serikali ikutunzie mtoto? Lazima na wewe uwe na bajeti yako!
Unajua biblia haisemi serikali leeni watoto, inaasema enyi wakina baba leeni watoto. Soma Waefeso 6:4. Sasa pale serikali itakapokusaidia wacha ikusaidie, lakini usikae unajiambia ya kuwa mimi nimezaa watoto kumi na tatu, lazima waende shule bure, lazima waende kwenye hospitali bure. Nani anayegharamia hizo huduma, unafikiri ni za bure? Hakuna! Wewe unaona huduma hizo ni bure, lakini yuko mtu ametoa pesa za kugharamia hizo huduma toka mahali fulani.
Nakumbuka wakati fulani nlikuwa Zimbabwe, baba mmoja aliyekuwa na cheo kikubwa tu kwenye makanisa ya kule Zimbabwe, tulikuwa tunazungumza naye siku moja juu ya masuala ya kusomesha watoto. Alisema wakati mmoja alikwenda Ujerumani kwenda kutafuta watu wa kuwasomesha watoto wake. Yule mzungu ambaye alikuwa anazungumza naye, akaamuuliza, “ndugu una watoto wangapi, akasema sita”. Akasema, “unajua mimi nina watoto wangapi.” Akasema, “sijui”. Akasema watoto wawili”. Akasema, “unajua ni kwa nini hatutaki kuzaa watoto wengi, usije ukafikiri tunachukia watoto, hasha ila ni kwa sababu ya gharama, za kuwatunza zilivyo kubwa”.Tunataka angalao kila mtoto atunzwe vizuri na aende shule nzuri, wakiishakuwa wengi nakuwa si rahisi kuwagharamia wote ipasavyo, na inabidi ugawe ulichonacho kidogo kidogo. Wanaishia wote shule ya msingi, kwa sababu huna hela ya kuwapeleka sekondari. Akasema, “sasa ninyi waafrika mambo yenu hayako sawa, wewe unaona mimi nimezaa kidogo nimejinyima kwa ajili ya watoto wangu wasome vizuri, sasa unataka fedha ya kwangu nikusomeshee watoto wa kwako ambao wewe umezaa bila kufikiria jambo la gharama ya kuwatunza wakiishazaliwa?”Aliambiwa kitu cha kweli usoni na mzungu! Unaweza ukafikiri alikuwa anamtukana, lakini alikuwa anamweleza kitu cha ukweli; watu wengi sana hawafikiri hiki kitu. Wale wazee wa zamani walikuwa wakizaa kwa mahesabu huku nyuma. Akizaa watoto wa kike wengi ana hesabu ng’ombe atakazopata watakapoolewa, usije ukafikiri ana hesabu gharama, bali ana hesabu ng’ombe atakazopata! Watoto wa kike kwake ni mradi. Akizaa watoto wa kiume anajua amepata nguvu kazi ya kulima mashamba, walikuwa wana mahesabu yao.
Lakini sasa hivi lazima ukae ufikiri kwa namna nyingine,sikuambii ya kwamba kuwa na watoto wengi ni kitu kibaya, ni uamuzi wako! Kama unataka kwenda na mstari unaohimiza mkaongezeke mkaijaze nchi (Mwanzo 1:28) hakuna shida! Unaweza ukaendelea na wewe ukawa kwenye kuijaza nchi, lakini usikazane kuijaza nchi halafu unataka wengine wakusaidie kulea watoto hao - hiyo sasa sio sawa!
Mimi sijui kwa upande wako, na sijui kwa upande wa wazazi wako, lakini ninakueleza ili baadaye uwe mzazi mzuri, ni vitu unahitaji kufikiri mapema. Niliwaambia watoto wangu siku moja, nikawaambia sikiliza, tumejiwekea maamuzi ndani ya hii  nyumba mimi na mama yenu, ya kwamba ni wajibu wetu kuwasomesha mpaka chuo kikuu ili angalau kila mmoja awe na shahada ya kwanza, huo ni wajibu wetu.
Baada ya shahada ya kwanza ukitaka kuendelea Mungu akubariki. Mungu akitupa nafasi ya kukusaidia kuendelea zaidi ya shahada ya kwanza tutakusaidia. Lakini tumemwomba Mungu atusaidie, kila mtu lazima afike chuo kikuu. Unajua kama usipoweka malengo ya namna hii, hata matumizi yako na bajeti yako haviwezi kukaa sawa. Ndio maana ninakuambia lazima umwombe Mungu akusaidie, usije ukafikiri kusomesha watoto ni kitu rahisi.

Ninyi mnajua ambao mko shule, wengine wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu wazazi wameshindwa kutoa karo za shule, na sio kwa sababu wanafunzi hawataki kuendelea na shule, lakini ni kwa sababu hakuna fedha za kuwasomesha.Nilimuuliza msichana mmoja katika mkoa mmoja wakati nilipokuwa huko kwa huduma, nikamuuliza “umemaliza darasa la ngapi”. Akasema, “kidato cha sita”. Nikamwambia, “sasa kwa nini hutaki kuendelea na shule?” Akanitazama usoni, halafu akasema, “sithubutu hata kumwambia baba anisomeshe zaidi maana ninawaangalia wadogo zangu huku nyuma walivyo na ninaangalia na hali ya baba yangu aliyonayo kifedha, amenisaidia nimefika kidato cha sita, sasa nikifikiria wadogo zangu – ambao bado wako shule za msingi, naona wacha na wao basi wasogee sogee angalau wafike sekondari na wao kama mimi. Kwa hiyo mimi nimenyamaza kimya”.Huyu msichana amemaliza kidato cha sita anataka kuendelea na masomo, lakini hawezi kuendelea kusoma kwa sababu anaangalia hali ya wazazi wake ilivyo, anajua kabisa angalau na wadogo zake na wao wasome, lakini sio kwamba anataka kuishia kidato cha sita.

No comments:

Popular Posts

Pageviews

WASILIANA NASI

Name

Email *

Message *