MAFUNDISHO
MAALUMU KWA VIJANA
By
Christopher
Mwakasege
Wiki
ya Pili
Jambo
la Pili
Unapoamua kuoa au kuolewa, fahamu ya
kwamba hiyo ndoa inakuunganisha na kukuingizakatika familia nyingine.
Unafahamu watu wengi sana wakioa au kuolewa wanafikiria tu mahusiano ya wao wenyewe tu; na hii ni hatari sana.
Unafahamu watu wengi sana wakioa au kuolewa wanafikiria tu mahusiano ya wao wenyewe tu; na hii ni hatari sana.
Kwa sababu unapooa unaingia kwenye undugu na
familia nyingine kabisa tofauti, na sio mahusiano ya kwenu tu wawili. Ninyi ni
kigezo tu cha kuunganisha hizo familia mbili, lakini mkiishaoana hizo familia
zenu mbili ni ndugu kuanzia wakati huo.
Ndio maana unapofika unataka kuoa au kuolewa, sio
suala la kumtazama kijana tu, au kumtazama msichana yeye mwenyewe tu; kwa mfano
alivyosoma, lakini ni lazima pia utazame na hali ya familia yake ili ujue
unajiingiza kwenye familia ya namna gani. Unapofika kwenye masuala ya namna
hiyo kuna vitu vingi sana vya kuangalia.
Unaweza ukaingia kwenye familia ambayo ni wavivu,
mimi ninakuambia jasho litakutoka ukioa msichana wa namna hiyo; au ukipata
kijana toka kwenye familia ya namna hiyo. Itakuwa kazi sana kumshawishi
mwenzako juu ya kujishughulisha na maisha. Maana inategemea; kwa kuwa unaweza
kuoa msichana hata kusonga ugali hajui. Sisi kwenye nyumba ya baba yetu, hatuna
msichana, tumezaliwa watoto wa kiume watupu, msichana wa kwanza kuingia kwenye
familia yetu ni mke wangu.
Lakini mama yetu alikuwa na bidii ya kutufundisha
kila kitu, alitufundisha kupika, alitufundisha kufuma, alitufundisha kusuka
nywele. Kwa hiyo nilijifunza kwanza kusuka tatu kichwa. Lakini sikuanzia
kujifunzia kusuka nywele kwenye kichwa cha mtu, bali nilijifunzia kwenye
majani; wao
wakikaa wanasuka hapo na sisi tuko hapo
tunafundishwa jinsi ya kusuka kwenye majani.
Sasa wengine hawapati nafasi ya namna hiyo, na ni
mbaya zaidi kwa wasichana. Mungu amenipa nafasi ya kuwa na watoto wakike watatu
na wa kiume mmoja, itakuwa ni aibu kwetu kama wazazi, ikafika wakati wanaingia
katika ndoa zao na hawajui kupika ni aibu; kwa hiyo lazima wajue kupika. Maana
kwa kujua hilo anaonyesha anatoka familia ya namna gani, na imemlea kwa namna
gani!
Unaweza ukafikiri unamlea mtoto wako vizuri, maana
siku hizi kuna shida ya kuwa na wafanya kazi majumbani mwetu. Ukishakuwa na
mfanyakazi nyumbani basi watoto wengine hawafanyi kitu, wakati mwingine
wanakula chakula na wanaacha sahani hapo hapo mezani.
Kuna watoto wengine inakuwa mpaka yuko sekondari
hawezi kufua nguo zake. Kwa kuwa nyumbani kama hakuna wa kumfulia basi kuna
mashine za kufulia. Huko unakokwenda kuolewa inawezekana hata mashine ya
kufulia hawajawahi kuiona! Unafika pale na unauliza mashine iko wapi,
wanakuambia yakufanyia nini, - ya kusagia mahindi? Maana ndio wanayoijua kuwa
ndio mashine!
Hujui hata namna ya kushika kioo cha taa ya chemli
wala namna ya kuiosha kule ndani lile vumbi likaondoka. Inawezekana mwingine
umezaliwa kwenye nyumba yenye umeme, lakini utakapokuwa katika ndoa unaenda
kwenye nyumba ambayo haina hata umeme, unafika kule na
unashangaa kweli maana hujui hata namna kuwasha taa
ya chemli! Kwa hiyo tunawaambia watoto wetu suala la kujifunza hivi vitu sio
suala la kuchagua, hata kama kuna mtu pale nyumbani wa kuwasaidia, ni lazima
wajue kufanya kazi!
Nilienda kwenye mkoa mmoja wakasema, sisi ukitaka
kuoa kwenye nyumba ya mtu, ukitaka kujua huyo msichana amelelewa vizuri au
vibaya wakasema usimtazame alivyovaa. Badala yake wanafika kwenye uwanja wa
nyumba ya wazazi wake, na wanaangalia ile barabara inayokwenda
nyumbani kwao, na wakiikuta chafu, basi wanajua
huyu msichana ni mchafu, hawahangaiki tena kuja kuzungumza, wanajua hapa kama
tunaamua kuoa tujue tunacho oa, huyu msichana ni mchafu!
Ukienda kuoa kwenye familia nyingine utakuta
wanasumbuliwa na ugonjwa wa kurithi, na usipojua kitu cha kufanya unaweza
ukapata shida sana. Lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba, uamuzi wa kuoa au
kuolewa unakuingiza kwenye familia nyingine kabisa, na inaunganisha hiyo
familia yao na familia yako; kwa hiyo hayo sio maamuzi madogo. Kumbuka unapooa
au kuolewa unawaingiza watu katika famila ambazo kama usipokuwa mwangalifu
inaweza ikaleta shida sana, lakini pia inaweza ikaleta baraka!.
Tutaendelea na mfulululizo unaofuata!
No comments:
Post a Comment