MAFUNDISHO MAALUM KWA VIJANA
By Mwalimu Christopher Mwakasege
Wiki
ya Tisa
Jambo la Tisa; Uko tayari kuoa au kuolewa lini, maana yake nimuda
gani ambao ungetaka kuoa au kuolewa?
Utasikia mwingine anasema, siku Mungu atakapo nipa
mume au mke, hii ni hatari
sana! Biblia inasema kwenye kile kitabu cha Mhubiri.3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.
sana! Biblia inasema kwenye kile kitabu cha Mhubiri.3:1 “Kwa kila jambo kuna majira yake na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”.
Kila kitu kilichoko chini ya mbingu kimeratibiwa,
kwa lugha nyingine, ni kwamba kila mwanadamu ana kalenda yake, iko kalenda yako
ya kuzaliwa, na ipo kalenda ya matukio na mipango mbalimbali. Mungu anaijua.
Mungu anatangaza mwisho tangu mwanzo, anajua mwisho wa maisha yako wakati wewe
unapozaliwa.
Katika mwanzo wa maisha yako, Mungu anakuwa
amekwishajua mwisho wako; utakavyokuwa; na kama amekwishajua mwisho wako, maana
yake ameshatembea kwenye maisha yako yote toka mwanzo mpaka alipofika mwisho,
na alipokamilisha maisha yako akarudi mwanzo ndipo akakuongoza kuzaliwa.
Mungu anapokuacha uzaliwe duniani, hakika ujue
kabisa ya kwamba amekwisha tembea na wewe katika maisha yako, amesharatibu
mambo yako na yako hatua kwa hatua; kwa mfano, kitu gani utafanya, wapi
utasoma, utasoma nini, utaolewa na nani au utaoa nani na itakuwa, lini, maisha
yako yatakuwaje, utamtumikiaje, mpaka mwisho wako. Akiishafika mwisho wa maisha
yako anarudi mwanzo, akishafika mwanzo anatangaza mwisho tangu mwanzo; kwa hiyo
kuanzia hapo unapozaliwa ujue maisha yako yote yamesharatibiwa!
Ni vizuri ufahamu hii mistari itakusaidia, maana
inakujengea msingi mzuri wa maisha hapa. Isaya.46:9-10 inasema,“Kumbukeni mambo
ya zamani za kale maana mimi ni Mungu wala hapana mwingine, mimi ni Mungu wala
hapana aliye kama mimi. Nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za
kale mambo yasiyotendeka bado, nikisema, shauri langu litasimama, nami
nitatenda mapenzi yangu yote”. Kwa lugha nyingine anatuambia ya kwamba, ‘wewe
unaona kila kitu ni kipya, unapoishi kila siku ni mpya, kila dakika inayokuja
ni mpya, Mungu anasema hiyo safari unayopita, mimi nilikwishaipita tayari,
nikafika mwisho wa maisha yako ndipo nikakuruhusu uzaliwe. Ulipokuwa unazaliwa
nikatangaza mwisho wako tangu wakati unazaliwa. Sasa mimi ninataka nikuambie
kama Mungu anajua, na shauri lake anasema litasimama katika maisha yako, ili
mapenzi yake ayatende katika maisha yako, unahitaji kuwa mwangalifu.
Kwa sababu kuna mpango na saa ya Mungu ya kuoa au
kuolewa, - ipo!Mungu anapokuletea mawazo ya kuoa au kuolewa, ni kwa ajili
yakuimarisha maisha yako na wito wako na kazi na makusudi, ambayo ameyaweka
hapa duniani. Atakuletea mtu atakaye imarisha wito wako, atakuletea mtu atakaye
saidiana na wewe, uwe ni mwanamke au uwe ni
mwanaume. Mungu anapo kukutanisha na mtu wa kuoana
naye ni kwa ajili ya kuimarisha nguvu zenu ili mtimize kusudi la Mungu. Kwa
hiyo lazima anajua kuna saa huyu mvulana anahitaji mke, au huyu msichana
anahitaji mume! Lakini watu wengi sana hawalifuatilii hili. Wakati sisi
tunaoana na mke wangu tulikuwa bado vijana, tulioana hatujafikisha hata miaka
thelathini, ninakumbuka nilikuwa na miaka 28. Tulijaliwa kuwapata watoto
tungali bado vijana sana. Lakini tuna watoto ambao ni wakubwa kwa sasa.
Tumefika kipindi ambacho tunaweza tukafuatilia masuala ya utumishi kwa namna
ambayo haiwaumizi watoto wetu sana!
Maana watoto wakiwa wadogo wote, mimi ninakuambia
kumtumikia Mungu ni kunakuwa kugumu sana, usije ukafikiri ni kurahisi. Maana
unahitaji kuwa karibu nao; wanahitaji kusoma shule, wanahitaji kufanya vitu
mbalimbali, wanahitaji kuwa na baba karibu, wanahitaji kuwa na mama karibu. Saa
nyingine mnataka kusafiri nao; unaweza ukasafiri nao lakini usije ukafikiri ni
kitu kirahisi.
Tulisafiri na Joshua (mtoto wetu wa nne) akiwa na
wiki sita. Sijawahi kuona watu wakisafiri na watoto wao wakiwa wadogo namna hiyo, Joshua
alikwenda kwenye huduma akiwa na wiki sita tu. Hatukuwa na namna ambavyo
tungeweza kumwacha. Sasa unaweza ukaelewa akiwa na wiki sita; maana yake mama
yake ana muda wa wiki sita tu tangu ajifungue na tulisafiri kwa gari, sio kwa
ndege, bali kwa gari!
Tulisafiri masaa karibu kumi na mbili, tumebeba kila
kitu, tumebeba mpaka unga wa kutengenezea uji, na beseni la kuogea, na maji.
Huwezi kumwogeshea mtoto mchanga wa wiki sita maji yoyote tu, kwa hiyo tulibeba
maji ya kumwogeshea. Huwezi kwenda ‘spidi’ unayotaka, ikifika saa yake ya kula
lazima usimame! Ukifika kwenye hoteli huwezi kumlaza jinsi unavyotaka, lazima uingie
kwanza uombe, uangalie yale mashuka yaliyoko halafu uombe, uangalie kile
kitanda halafu uombe, uangalie kila kitu kule ndani halafu uombe!
Wewe ni mtumishi wa Mungu, ukienda na mtoto kienyeji
kienyeji tu, ibilisi anaweza akamvamia na ukapata shida, na huduma yako yote
uliyoiendea ikaharibika. Unaweza ukatamani saa nyingine usinge- safiri naye.
Lakini mnaposafiri pamoja, kumbuka ina gharama yake.
Lakini mambo haya unahitaji kufiri mapema, ili uweke
kwenye agenda yako ya maombi ujue kabisa mpango wa Mungu ya kuwa unatakiwa kuoa
au kuolewa lini. Ninajua kwa wengi kinakuwa kigumu hicho, maana wengine
wametamani kuolewa jana, hawajapata wanaume, wengine wangetaka kuoa leo, lakini
bado hawajapata msichana wa kuoa.
Wengine wanatamani kuolewa si kwa sababu mpango wa
Mungu umefika wa kuolewa; ila ni kwa sababu wanaona muda wao wa kuolewa
umefika, wengine wanaona umri umesogea. Mpango wa Mungu juu ya maisha yako,
haubabaishwi na jinsi wewe unavyohesabu miaka,jirani zako wanavyohesabu miaka,
ndugu zako wanavyohesabu miaka, au rafiki zako wanavyohesabu miaka.
Mungu anajua alichopanga kwa ajili yako, ana
kalenda yako kabisa, na kila alichokichagua Mungu ndicho sahihi.
No comments:
Post a Comment