MAFUNDISHO MAALUM KWA VIJANA
By
Mwalimu Christopher Mwakasege
Wiki
ya Nane
Jambo la Nane; “Je! Uko tayari kuolewa na nani”
Wengine hawafikirii namna hiyo, ukiwauliza uko
tayari kuolewa na nani, anasema na mtu
aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri, unataka kuolewa na nani.
aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka, wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri, unataka kuolewa na nani.
Labda hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo,
nataka nikufikirishe vitu vya kawaida kabisa.
Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na mtumishi, hesabu
gharama kwanza! Wengine wanaona tunavyoshirikiana na mke wangu katika huduma wanamtazama
wanasema, wanataka kuolewa na mtumishi; kaamuulize mke wangu, tulipokutana hata
wito haukuweko, na tulikutana wote hatujaokoka. Tulikuja kuokoka baada ya
kuoana! Mungu ametuteremshia utumishi tuko kwenye ndoa tayari, kwa hiyo
usitamani ndoa ya kwetu, tamani ya kwako ambayo Mungu amekupangia. Mke wangu
hakunipendea utumishi, sikuwa na tone la utumishi, wala hata ya kufanania ya
kwamba nitaokoka, na yeye alikuwa
hajaokoka pia wakati huo. Lakini kwa saa na kwa makusudi na kwa utaratibu wa Mungu,
tumekuwa jinsi tulivyo. Akatuteremshia utumishi wakati tumekwishaokoka na
tumekwishaoana!
Usijaribu kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu
mwingine, hujui iliko toka, tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka
mtumishi, lakini watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna
gani? Lazima ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka mhubiri,
hata nabii ni mhubiri, mwinjilisti ni muhubiri,
mwalimu anaweza akahubiri. Kitabia hawafanani, haleluya! Nataka nikufikirishe
ikusaidie, maana nataka nikujengee msingi mzuri wa maisha ambao ukikanyaga
vizuri shetani alie tu, maana hatawezi kukuvuruga.
Maana watu wengi wanapata shida sana wanapotaka
kuoa au kuolewa, utakuta wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na mtumishi,
hayo ni maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya
Roho Mtakatitu, bado yuko chekechea, unajua lazima
uwe ‘very specific’. Mungu anataka useme naye kile kitu unachokisikia ndani
yako. Anajua kabisa kitu ambacho ni kizuri kwa ajili yako; lakini Mungu hataki
kukulazimishia tu, anataka ushirikiane naye, ili akikupa kitu ukipokee kwa
furaha.
Kwa hiyo kama unataka mtumishi, ni muhimu useme
unataka mtumishi wa aina gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu
gharama, lazima uwe na neema ya kukaa na mwinjilisti.
Si unajua mwinjilisti hakai nyumbani, anazunguka,
akikosa watu wa kuwachapa injili huko nje, anakuja kuchapa injili nyumbani hata
kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi kumaliza ibada ya jioni mpaka awepo mtu wa
kutubu, hajatubu ataendelea kufanya maombi. Kama hauko tayari kuchukuliana na
mtu wa namna hiyo usiamue kuoa au kuolewa naye.Lazima useme; au kama unataka
kuolewa na nabii jipange, kwa sababu hajui kuongea na watu, muda wake mwingi
yuko kimya, manabii mara nyingi wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya.
Mara nyingi amejifungia kuomba peke yake na Mungu. Hata saa nyingine unatamani
uombe pamoja naye, lakini Mungu anataka yeye peke
yake. Wewe nenda kwenye biblia utaona maisha yake yalivyo kila kitu
kinachomzunguka, kila kitu anachovaa, kila kitu anachokutana nacho,
Mungu anaweza akakigeuza ujumbe. Kwa hiyo usije
ukashangaa kesho akakutazama na akaishia kupata mahubiri toka kwako, halafu
mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na unamuuliza sasa wewe ulikuwa
unanihubirije?
Kwani wewe hukujua ya kwamba ni nabii na anaweza
kupata ujumbe unaosema: “kama vile mke wako alivyovaa, ndivyo na kanisa langu
lilivyo asema, Bwana”! Wewe usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na
anaona jinsi mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu, “kama
vile mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto,
ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili ya watoto wangu, asema Bwana”! Saa
nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani vinaonekana, ujumbe unatoka
saa hiyo mara moja, anasema, “Kama vile mke wako alivyovaa nguo iliyopasuliwa
na watu wanaona ndani, ndivyo na kanisa langu lilivyo vazi lake limepasuliwa na
shetani anaona ndani”! Lazima uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na
nabii. Uwe tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii! Unataka
kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea wageni. Mwingine anasema
mimi ninataka kuolewa na mtumishi lakini ndani yake anawaza mtu anayezunguka na
kuhubiri, kumbe Mungu ameweka ndani yake mtumishi, lakini ni mfanya biashara. Mfanya
biashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio sehemu yake kumtumikia
Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni dereva, wanapakwa mafuta sehemu
zao hizo za utumishi, usije ukafikiri hao wanaoafanya kazi nyingine sio
watumishi wa Mungu. Mungu anawapaka mafuta kwa ajili ya hizo kazi, ili
walitumikie kusudi lake. Kwa hiyo unapokwenda katika maombi unasema tu mimi
ninaomba mtumishi, Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine
wanafagia barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye vyoo
vya kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha nyumba za watu, nao ni watumishi
wa Mungu,oh haleluya! Mungu akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi
sikuomba huyu niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu,
usimnenee kitu cha namna hiyo. Kama msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu,
au kijana ni mrefu unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi
kukupa, lakini wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine anakuwa mfupi kiasi
ambacho anafanana kama vile ni mtoto kwako, wenzako wanakuuliza tangu lini
umepata mtoto na akakua na akawa mkubwa namna hii, unasema “ninyi msiseme
hivyo, ni mume wangu huyu”. Ni uamuzi wako. Sasa, si lazima mfanane urefu,
lakini msipishane sana; kwa kweli ni kwa faida yenu wenyewe, haleluya!Kama
msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana unaweza ukapata mtumishi
wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe huzitaki. Ikifika siku umeingia tu kwenye
ndoa kitu cha kwanza unamtafutia wembe ili anyoe ndevu zake – hii ni kumwonea!
Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe wewe ulikuwa unamtegea tu ili baada ya arusi tu
umpe wembe! Wako wasichana wanaopenda wanaume wenye ndevu, waachie hao! Huyu
Bwana Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa ninawaza jinsi Mungu alivyomuumba
mwanadamu na nabaki ninashangaa sana. Maana kuna wanaume wengine hata ndevu
hawana, hata wakilazimishia kunyoa kidevu kitupu haziji. Sasa mtu mwingine
anajisikia vibaya, akifikiri ya kuwa mtu anaonekana ya kwamba yeye ni mwanaume
kwa sababu tu ana ndevu, si kweli. Kuna wanaume wengine wametengenezwa namna
hiyo ‘special’ kwa ajili ya wasichana wasiotaka wanaume wenye ndevu, haleluya! Maana
mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka karibu na kwenye pua. Sasa kama
ni mtu mweusi sana ‘ni hatari sana’, giza likiingia tu ndani ya nyumba wewe
unamwambia ‘cheka’, akicheka yale meno yake yanaweza yakamulika kidogo, na
utajua yuko wapi! Hivi vitu ukishaingia kwenye ndoa ni vitu vikubwa sana,
kuliko watu wanapoviangalia kabla hawajaoana. Wewe unakuta kijana anaoa
msichana ana rangi nyeusi nzuri tu, akifika ndani unamletea madawa ajikoboe,
wewe ulikuwa unamwoa wa nini? Hiyo sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli
nimechukua tu huyu, lakini sio niliyekuwa namtaka! Niliyekuwa namtaka ni
mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha nimkoboe mpaka afike rangi ninayotaka,
- haviendi namna hiyo bwana! Mungu alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo
aliona, alimtazama alivyo na weusi wake huo akaona kila kitu chema, akajipa sifa,
akajipa maksi asilimia mia moja, amefanya kitu chema! Sasa akitaka kupaka rangi
hiyo ‘nyumba yake’ na kuinakshi ni kitu kingine. Unajua kuna nyumba nyingine
hazipendezi mpaka uzipake rangi fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine
hawawezi kupendeza mpaka wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa utapata
mtihani mgumu, nimeona, kijana anampenda msichana, lakini msichana anaweka
rangi kwenye midomo yake, kucha zake anaweka rangi, anachora na kalamu hapa
kwenye nyusi kidogo, ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu
kingine juu ya uso wake. Umempenda akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia
hukumuuliza hayo maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo
rangi! Hiyo ni kumwonea, maana ulimkuta akiwa hivyo, kama ulikuwa humtaki akiwa
amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa kumfuatilia, wako wengine ambao watakuwa
radhi na huyo anayejipaka rangi! Kuna kijana alioa msichana, wamefika ndani
wakaanza kugombana naye habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, - nywele tu!
Huyu dada kaenda katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki. Lakini
alimkuta yule msichana anatengeneza nywele kwa staili hiyo, sasa kwa nini hivi
vitu hawakutaka kuzungumza kabla ya kuamua kuoana? Mimi ninataka nikusaidie
upunguze ugomvi ndani ya ndoa utakayokuwa nayo; maana vitu ambavyo Mungu
atawaletea vya kufanya pamoja kwenye ndoa ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi
ambacho hamhitaji kutumia muda wenu kushindania vitu vidogo vidogo ambavyo
mlikuwa muwe mmekwisha kuvijadili kabla ya kuoana. Mna mambo muhimu sana ya
kufanya, kiasi ambacho kuanza kushindana na kubishana juu ya vitu ambavyo mlitakiwa
muwe mumeshavizungumza kabla ya kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa Mungu
ulivyo juu ya kumpata mwenzi wa maisha.
1 comment:
AMINA nimepata vitu vingi mnooo barikiwa sana Baba
Post a Comment